Hakiki riwaya ya Fedheha kwa kigezo cha nadharia, fani na maudhui.
SWALI: Hakiki riwaya ya Fedheha kwa kigezo
cha nadharia, fani na maudhui.
UHAKIKI
WA RIWAYA YA FEDHEHA
Jina
la kitabu Fedheha linasadifu yaliyomo kwani kwa tafsiri ya kawaida neno fedheha
linamaanisha aibu aipatayo mtu. Kwa hali hiyo basi jina la kitabu linaendana na
yaliyomo kama ifuatavyo:-
·
Khalfani alifedheheshwa baada ya
kujulikana/ kusemekana sababu iliyopelekea kwenda mahabusu ni kukutwa na shoga
nyumba ya kulala wageni. (Uk. 62)
·
Fedheha nyingine ilijitokeza pale Baisar
uovu wake ulipobainishwa na kuwekwa wazi kuwa alijihusisha na uuzaji na
usafirishaji wa madawa ya kulevya na kumiliki danguro. (Uk. 87, 105-106)
·
Pia Khalfani alifedheheshwa na mkewe Latipha
kuolewa na Baisar. Vilevile Baisar kumtumia Latipha kusafirisha madawa ya
kulevya. (Uk.36)
·
Fedheha nyingine inaonekana kupitia mama
yake Khalfani baada ya kusukumwa na askari mbele ya mwanae na kuanguka chini.
(Uk. 29)
Utangulizi
Riwaya
hii ya Fedheha imeandikwa na George Iron Mosenya, kwa ujumla inahusu mkasa wa
kimapenzi kati ya Khalfani Masoud na Latipha ambapo mkasa huu wa kimapenzi
unaibua masuala mengine mazito kama uuzaji wa madawa ya kulevya, usaliti katika
ndoa na umiliki wa biashara ya danguro.
Ufuatao
ni uhakiki wa riwaya ya fedheha kwa kutumia kigezo cha fani na maudhui.
Maudhui
1. Dhamira
kuu.
Mapenzi
na ndoa, dhamira hii kwa sehemu kubwa imepelekea kuibuka kwa masuala mengine yaliyojadiliwa
na mwandishi katika riwaya hii. Pia mwandishi ameonesha kuwepo kwa mapenzi ya
kweli na yasiyo ya kweli.
Mapenzi
ya kweli yanajitokeza kati ya Khalfani Masoud na Geza Ulole ambapo Geza
alikubali kutumia muda wake mwingi kutatua tatizo lililokuwa linamkabili
Khalfani katika kujua ukweli juu ya mke wake Latipha
Mapenzi
mengine ya dhati yanajitokeza pale Geza Ulole anapoonesha moyo wa uzalendo
baada ya kuwaokoa abilia wenzake wakati walipotekwa na majambazi. (Uk. 38)
Khalfani
alionesha mapenzi ya dhati kwa Latipha.
Mapenzi
yasiyo ya kweli mwandishi anayabainisha kupitia Latipha kwa Khalfani. (Uk. 16)
Latipha
kuolewa na bwana mwingine. (Uk. 34)
Pia
Lolita kumsaliti Geza Ulole.
Dhamira
ndogondogo.
i.
Usaliti,
Mwandishi
ameonesha jambo hili kupitia mhusika Latipha kumsaliti Khalfani kwa kuolewa na
Baisar (Uk. 16). Vilevile usaliti mwingine unajitokeza kupitia mhusika Lolita
kumsaliti mpenzi wake Geza Ulole kwa kuolewa na mwanaume mwingine.
ii.
Rushwa,
Suala
hili limejitokeza baada ya Geza kutoka gerezani na kukuta mama yake amekufa na
chanzo cha kifo chake ni kuwa mwarabu (Baisar) amehusika (Uk. 60 na 87)
iii.
Uongozi mbaya,
Suala
hili limejitokeza kupitia vigogo wakubwa wa Serikali pamoja na vyombo vya dola
ambapo walishirikiana na wahalifu kuwatesa wanyonge (Uk. 60) mwandishi amesema
kuwa Baisar alikuwa na pesa, pesa hizo alizifanya fimbo kwa wanyonge. (Uk. 87)
iv.
Biashara haramu,
Suala
la madawa ya kulevya, jambo hili limebainishwa na mwandishi anapomtumia mhusika
Baisar kuwa alikuwa akijihusisha na biashara hiyo kwa kutumia mabinti. (Uk. 87,
105)
Suala
la uuzaji wa miili (Danguro), mwandishi ameonesha kuwepo kwa biashara ya uuzaji
wa miili ya wasichana maskini ambapo ilimilikiwa na Baisar. (Uk. 87)
v.
Uvumilivu,
Mwandishi
ameonesha dhamira hii kupitia mhusika Khalfani kwani ameonesha uvumilivu wa
hali ya juu kulinda penzi lake kwa Latipha (Uk. 36)
vi.
Matabaka,
Mwandishi
amebainisha kuwepo kwa suala hili la walionacho na wasionacho kama mke wa
Baisar alipotekwa vyombo vya habari vilitangaza lakini watu wengine walipotekwa
kama Latipha hakuna aliye andika habari hii kwa kuwa wao ni maskini. (Uk. 76)
vii.
Wivu,
Mwandishi
kaonesha kuwepo kwa dhamira hii akimhusisha mhusika mkuu Khalfani kuonesha hali
ya wivu juu ya mkewe Latipha, wakati aliposikia mlio wa simu ya mke wake kwenye
daladala. (Uk. 2)
viii.
Umoja na mshikamano,
Dhamira
hii imebainishwa kwa kuwatumia wahusika Khalfani na Geza Ulole waliposhirikiana
tangu walipo fahamiana na haatimaye kupelekea kupatikana kwa Latipha na kufungwa
kwa Baisar na mke wake. (Uk. 31)
ix.
Ujasiri na kujitoa mhanga,
Mwandishi
amebanisha kuwepo kwa dhamira hii kwa kumtumia Geza Ulole alipojitoa mhanga kwa
kuwaokoa abiria wenzake wakiwa safarini toka Mwanza kuelekea Dar es
Salaam. (Uk. 38)
x.
Ukosefu wa haki,
Mwandishi
amejadili dhamira hii kupitia mhusika Khalfani akionesha kutuhumiwa kwa kesi
asizozifahamu pia hakupewa muda wa kujitetea. (Uk. 29)
xi.
Nafasi ya mwanamke katika jamii,
Mwandishi
amemchora mwanamke katika nafasi mbalimbali kama:-
Msaliti
wa ndoa, mwandishi amemtumia Latipha katika suala hili.
Kama
mlezi, mwandishi amemuonesha mhusika mama Latipha kama mama mwenye malezi
mabaya katika kumlea mwanae Latipha.
Vilevile
mwandishi amemuonesha mama Khalfani kama mama mwenye malezi mabaya na asiye
penda kusikiliza maelezo yoyote kutoka kwa mwanae Khalfani.
Mwanamke
amechorwa kama chombo cha starehe, kwa kumuonesha mama Latipha kumstarehesha
Baisar.
Mwandishi
amemwelezea mwanamke kama mwenye kushiriki uovu, msanii ameonesha haya kwa
kumtumia mhusika Mozah kuonekana akishirikiana na mume wake (Baisar) kumtunzia
siri.
Kama
jasiri, mtunzi ameonesha haya kwa kumtumia mke wake Baisar alipopambana na
Khalfani kama njia ya kujiokoa nyumbani kwa Geza.
Kama
msomi, kwa kuwatumia Latipha na Mariamu kuwa ni wanafunzi wa Chuo Kikuu.
Asiye
na msimamo, mwandishi amebainisha hili kupitia mhusika Latipha hakuwa na msimamo
wa kuitetea ndoa yake na kuamua kuolewa na Baisar.
Kama
mwongo, mwandishi amemwonesha Latipha akimdanganya mume wake Khalfani kuwa
anataka kugombea mashindano ya umiss Chuo.
2. Ujumbe.
i.
Umoja na ushirikiano ni nguzo bora
katika utatuzi wa matatizo mbalimbali.
ii.
Ni vizuri kupembua ushauri tunaopewa na
ndugu na jamaa zetu.
iii.
Usaliti kwa wanandoa na wapenzi haufai
na mwisho wake ni mbaya.
iv.
Ni vizuri kujiepusha na biashra haramu
(Uuzaji wa madawa ya kulevya na umiliki wa danguro)
v.
Ni vizuri kumsikiliza mtoto katika
matatizo yanayomkabili.
vi.
Unapotafuta haki yako usikate tamaa.
vii.
Ofisi na taasisi za umma zitende haki bila
kujali tofauti zetu.
viii.
Usilazimishe mapenzi kwa mtu asiye
kupenda.
ix.
Wivu kupita kiasi katika mapenzi haufai
x.
Si vizuri kwa wazazi kuchangia kuvunja
ndoa za watoto wao.
xi.
Mwanaume ni kiungo muhimu katika
familia.
3. Falsafa.
Mwandishi
anaamini kuwa, ili jamii yoyote iweze kuwa na mabadiliko chanya na yenye usawa
kwa wote, ni lazima iondokane na mambo yote yanayokwamisha ujenzi wa jamii mpya
endelevu kama:- Rushwa, uuzaji wa madawa ya kulevya, usaliti, malezi mabaya na
ubaguzi.
4. Msimamo.
Msanii
anamsimamo wa kiyakinifu kwani ameyabainisha matatizo yanayoikabili jamiii
kama:- usaliti, uuzaji wa madawa ya kulevya,
uuzaji wa miili (danguro) na pia ameonesha njia za utatuzi wake kama
kushitakiwa na kufungwa kwa Baisar na mke wake.
5. Mtazamo.
Mwandishi
anamtazamo wa kimapinduzi kwani ameonesha na kubanisha mapambano na mgongano wa
kitabaka uliopo kati ya tabaka la juu na tabaka la chini, mambo ambayo ni
halisi katika jamii zetu.
6. Itikadi.
Mwandishi
ameegemea kwenye jamii yake kwani ameonesha mambo mbalimbali yanayolikabili tabaka
tawaliwa kama vile suala la rushwa,uongozi mbaya, unyanyasaji na uuzaji wa
madawa ya kulevya.
Fani.
1. Muundo.
Muundo
hujimwisha sura, msuko, mandhari na wahusika.
i.
Sura,
Mwandishi
wa riwaya hii amegawanya kazi yake katika sura kumi na tisa (19). Sura ya 1-3 zinazungumzia
mapenzi na ndoa ya Khalfani Masoud na Latipha, wivu na migogoro ya ndoa kati yao.
Sura ya 4 - 6 zinazungumzia kupotea kwa Latipha, kukamatwa kwa Khalfani,
kupelekwa mahabusu na kutolewa kwake. Sura ya 7 – 9 Geza na Khalfani
kusimuliana mapito yao, kwenda ukumbini kubainisha/ kutafuta chanzo cha tatizo.
Sura ya 10 -13 kubainisha adui yao na kupanga mbinu za kupambana naye. Sura ya 14 – 16 kupanga mipango ya kuingia kwa Baisar,
kumteka mke na watoto wake. Sura ya 17 – 19 kurudi tena kwa Baisar kutoa
vitisho, kupambana na Baisar na hatimaye Baisar na mkewe kufungwa.
ii.
Msuko,
Mwandishi
ameonesha mpangilio wa visa na matukio ni wa moja kwa moja kwani anabainisha
tangu matukio yanaanza mpaka yanakamilika. Mwandishi ameonesha Khalfani anaanza
mahusiano na Latipha, ndoa yao, Khalfani kwenda mahabusu, kukutana na Geza
Ulole, kutafuta mbinu za kupambana na Baisar, kumpata Latipha na kufungwa kwa
Baisar na mke wake.
iii.
Mandhari,
Mazingira
halisi ya Kitanzania, mandhari ya Dar es Salaam, Mwanza na Morogoro.
·
Dar es Salaam muktadha wa Koko beach
(Uk. 7) Mbezi Africana (Uk. 82), Temboni, Chuoni (Chuo cha Uhasibu), Hospitali
ya Magomeni (Uk. 25), kwenye daladala
(Uk. 3).
·
Mwanza muktadha wa mahabusu (Uk. 31 na
38).
·
Morogoro muktadha wa nyumba ya kulala
wageni (Uk. 100).
iv.
Wahusika,
Khalfani.
Ø Mhusika
mkuu.
Ø Mume
wa Latipha.
Ø Mwenye
wivu kwa mkewe.
Ø Jasiri.
Ø Mvumilivu.
Ø Ana
mapenzi ya dhati kwa mkewe.
Ø Msomi
wa Chuo Kikuu.
Ø Mtoto
wa mama Khalfani.
Ø Anafaa
kuigwa na jamii.
Geza
Ulole ( Iga ufe).
Ø Rafiki
wa Khalfani.
Ø Mtu
wa kisasi.
Ø Jasiri.
Ø Mvumilivu.
Ø Mshauri
mzuri.
Ø Mbabe (Uk. 31)
Ø Alikuwa
mpenzi wa Lolita.
Ø Anafaa
kuigwa kwa baadhi ya mambo.
Latipha.
Ø Mke
wa Khalfani na Baisar.
Ø Hana
mapenzi ya kweli kwa Khalfani.
Ø Msomi
wa Chuo Kikuu.
Ø Msaliti
wa ndoa.
Ø Mwongo.
Ø Msafirishaji
wa madawa ya kulevya.
Ø Hafai
kuigwa na jamii.
Baisar.
Ø Ni
mume wa Mozah Baraghashi.
Ø Baba
wa watoto wawili.
Ø Mwarabu.
Ø Mfanyabiashara
wa madawa ya kulevya na mmiliki wa danguro.
Ø Anashirikiana
na vigogo Serikalini kuumiza wanyonge.
Ø Malaya.
Ø Hafai
kuigwa na jamii.
Mama
Latipha.
Ø Mama
mzazi wa Latipha.
Ø Alishiriki
kuvunja ndoa ya bintiye.
Ø Ni
hawala wa Baisar.
Ø Mama
mkurupukaji.
Ø Ana
vitisho.
Ø Hafai
kuigwa na jamii.
Mama
Khalfani.
Ø Mzazi
wa Khalfani.
Ø Hapendi
kumsikiliza mwanae.
Ø Hachambui
kila anachokisikia.
Ø Hafai
kuigwa na jamii.
Wahusika
wengine ni kama:- Mariam, Lolita, Jemsi, John na Michael.
2. Mtindo.
Mbinu
za kiuandishi.
·
Mwandishi ametumia herufi kubwa kwa kila
neno la kwanza mwanzoni mwa kila sura.
·
Ametumia mbinu ya masimulizi na kwa
sehemu chache ametumia mbinu ya majibizano. Mfano, Majibizano kati ya Khalfani
na Baisar (Uk. 98), majibizaqno kati ya Geza na Khalfani (Uk. 51).
·
Pia mwandishi ametumia mbinu ya ndoto katika
kazi yake, ambapo ndoto hiyo iliotwa na Khalfani (Uk. 20- 21).
Matumizi
ya lugha.
Kwa
ujumla lugha iliyotumiwa na mwandishi ni nyepesi, fasaha na yenye kueleweka kwa
wasomaji wake. Yafuatayo ni matumizi ya lugha kama yalivyojitokeza katika
riwaya hii:-
i.
Misemo.
Baadhi
ya misemo iliyojitokeza ni kama:-
a) Mapenzi
yananipeleka puta (Uk. 2)
b) Funika kombe mwanaharamu apite (Uk. 7)
c) Mtu
mzima dawa (Uk. 8)
d) Kulivalia
njuga (Uk. 8)
e) Mtoto
hakui kwa mamae (Uk. 28)
f) Kutwanga
maji kwenye kinu (Uk. 20)
g) Usihukumu
ladha ya kitabu kwa kutazama jalada lake (Uk. 65)
h) Vizuri
huliwa na wengi (Uk. 41)
i)
Umbali hunyausha mapenzi (Uk. 9)
ii.
Methali.
a) Hayawi
hayawi hatimaye yakawa (Uk. 8)
b) Mkuki
kwa nguruwe kwa binadamu mchungu (Uk. 84)
iii.
Nahau.
a) Nikaukata
mzizi wa fitina (Uk. 23)
b) Niko
chini ya miguu yako (Uk.28)
c) Yule
boya hana kifua (Uk. 81)
d) Kukata
shauri (Uk. 39)
e) Bega
kwa bega (Uk. 84)
Tamathali
za semi
i.
Tashibiha,
a) Aliendelea
kuwa mbele na mimi nyuma kama mkia (Uk. 49)
b) Moyo
ukipiga hodi kwa nguvu kifuani kama unaosisitiza kuwa unataka kutoka nje
kupunga upepo (Uk. 37)
ii.
Tashihisi,
a) Harufu
iliyonipokea pale iliupasua moyo wangu kwa hofu (Uk. 3)
b) Nilifumba
macho nikauma meno yangu kisha nikaitazama mikono yangu jinsi ilivyo shindana
kutokwa jasho (Uk. 14)
c) Ile
hasira ikaondoka na uwoga wangu (Uk. 71)
d) Kauli
hizi zilizopita katika kichwa changu ziliniumiza sana kiasi kwamba niliusikia
moyo ukipiga hodi kwa nguvu kifuani kama unasisitiza kuwa unataka kutoka nje
kupunga upepo (Uk. 37)
e) Mkojo
ukabisha hodi (Uk. 74)
iii.
Tashititi,
a) Latipha
mke wangu una wazimu, nikamuuliza huku nikimtazama usoni (Uk. 12)
b) Huyu
ndiye mume wake ama? (Uk. 42)
c) Waliniona
nimekabwa kisha nikapigwa vibaya sana, halafu wananiuliza kitu gani kimetokea
(Uk. 26)
iv.
Tafsida,
a) Michael
huku akiondoka kuelekea msalani (Uk. 5)
b) Mambo
yaliyokuwa yanafanywa nao wakiwa faragha (Uk. 7)
v.
Misimu,
a) Kesho
kitanuka mjini hapatakalika (Uk. 76)
b) Zoba
(Uk. 60)
c) Boya
(Uk. 81)
vi.
Kejeli,
a) Marashi
gani hayo nimeyapenda sana nilimsanifu (Uk. 11)
b) Kina
Latipha wapo wengi au kesho nikuletee Latipha mpya uoe fasta fasta Geza
alinihoji kimasihara huku nikicheka (Uk. 45)
Mbinu
za kisanaa.
i.
Takriri,
a) Kilevi
levi (Uk. 5)
b) Kimya
kimya (Uk. 3)
c) Ama
hakika dhaifu ni dhaifu tu (Uk. 90)
d) Fasta
fasta (Uk. 45)
e) Geza
alikoroma, alikoroma,alikoroma (Uk. 90)
f) Nikawa
nikibofya bofya simun yangu (Uk. 38)
g) Mimi
namuua, namuua nasema (Uk. 88)
ii.
Mdokezo,
a) Wanaume
wengine ……… yaani mimi kaka nikija …… (
Uk. 7)
b) Halafu
umesema uponaye katika dili gani we si ulise …….. (Uk. 50)
c) Baisar
na …… na ……. (Uk. 77)
d) Huyu
bwana anaratibu mashindano ya urembo kisha …… kisha ….. (Uk. 22)
iii.
Nidaa,
a) Geza
alikuwa anamiliki gari!! (Uk. 67)
b) Nikahangaika
huku na kule!!! (Uk. 15)
c) Hakuwa
Gezaa Yule hakika!! (Uk. 67)
iv.
Matumizi ya lugha ya kiingereza.
a) Delete
yes ……. No ……. (Uk. 81)
b) One
million (Uk. 4)
c) Any
way (Uk. 59)
d) I’m
sorry (Uk. 11)
e) Big
up (Uk. 73)
v.
Matumizi ya lugha ya Kiarabu,
Wallah
(Uk. 53)
UHAKIKI
KWA KUTUMIA NADHARIA YA UHALISIA
Mambo
ya msingi katika nadharia ya uhalisia yaliyojitokeza katika riwaya hii ni pamoja
na:- lugha rahisi isiyofikirisha,
wahusika, matukio mahususi, ukweli, hakuna ufundi mkubwa wa kifani na
demokrasia.
Lugha
rahisi isiyofikirisha, lugha aliyotumia mwandishi ni lugha rahisi na yenye
kueleweka kwa wasomaji kwani hajatumia lugha ya picha au ya mficho, viwango vyote
vya elimu wanaweza kusoma na kuelewa.
Wahusika,
msanii ametumia wahusika wanaosadifu uhalisia katiak jamii. Mfano, kama
Khalfani na Latipha katika mapenzi yao, suala la usaliti lililojitokeza kwa
latipha katika jamii yetu ya leo wapo watu kama hao. Pia Khalfani anawakilisha
watu wenye mapenzi ya dhati katika jamii ya leo, hivyo mwandishi ametumia
wahusika wenye kuonesha uhalisia.
Matukio
mahususi, mwandishi ameyapangilia matukio katika uhalisia kutokana na kuwa
matukio yaliyojitokeza katika riwaya hii ni kama vile utekaji wa gari, Khalfani
kupelekwa mahabusu bila kuelewa kosa lake, kupewa kichapo na ndugu wa Latipha,
kutekwa kwa mke wa Baisar na watoto ambapo mambo kama haya yanawakumba watu
katika jamii yetu ya leo.
Ukweli,
mwandishi wa riwaya hii ameonesha ukweli kuanzia mwanzo hadi mwishoni mwa
riwaya hii ya fedheha, kwani mambo yaliyojitokeza kama vile:- rushwa,
kubambikizwa kesi, usaliti, wivu kupita kiasi katika mapenzi na usafirishaji wa
madawa ya kulevya ndivyo yalivyo katika jamii yetu ya leo.
Demokrasia,
suala la haki kwa kiasi limejitokeza katika riwaya hii mfano, baada ya Baisar
kuainisha wazi mambo yake aliyokuwa anawafanyia wananchi, alipelekwa mahakamani
na kufungwa kifungo cha maisha. (Uk. 106)
Haukuna
ufundi mkubwa wa kifani, wanauhalisia wanalenga zaidi kipengele cha maudhui
kuliko fani kwani maudhui hulenga zaidi mambo yanayojiokeza katika jamii. Hivyo
basi riwaya hii imelenga zaidi maudhui kuliko fani.
Kwa ujumla riwaya hii
ya Fedheha imesadifu hali halisi ya maisha ya Tanzania, kutokana na mambo
yaliyojadiliwa na matokeo ya mambo hayo. Hivyo mwandishi wa riwaya hii amefaulu
kwa kiasi kikubwa kuakisi maisha ya nchi zinazo endelea hususani Tanzania.
Comments
Post a Comment