Ijue falsafa ya kiafrika katika fasihi simulizi
Kazi hii imegawanyika
katika sehemu kuu tatu ambazo ni utangulizi kiini na hitimisho.Katika
utangulizi kuna maana ya falsafa fasihi simulizi na
FALSAFA YA KIAFRIKA
Falsafa ni dhana ambayo imefasiliwa na watu tofautitofauti kwa mitizamo ambayo hulenga katika kumaanisha
kitu kimoja.Wataalamu mbalimbali wametoa mawazo yao kuhusu dhana hii ya falsafa
kwa kutoa maana mbalimbali.Wafuatao ni wataalamu na maana za falsafa na falsafa
za kiafrika.
Falsafa
(kutoka Kigiriki filosofia = pendo la hekima) ni jaribio la
kuelewa na kueleza ulimwengu kwa kutumia akili
inayofuata njia ya mantiki. Wamitila, K.W. (2003).
Neno
Falsafa hutokana na maneno mawili ya kiyunani yaani philo lenye
maana ya upendo na Sophia
linalomaanisha hekima.
Hivyo utaona kuwa falsafa ni Taaluma
inayojishughulisha katika kutafuta ukweli wa jambo kwa njia ya kutafakari.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa
falsafa ni taaluma inayo dadisi hali halisi ya maisha ya binadamu kwa kuzingatia
imani, mila, desturi, pamoja na mienendo aliyonayo binadamu katika jamii yake,
huku akitafakari njia sahihi na bora za kuweza kutatua changamoto mbalimbali
anazo kabiliana nazo katika maisha yake ya kila siku.
Maana ya fasihi;
Ngure(2003) anasema kuwa fasihi ni aina ya sanaa ambayo wasanii
wake huonyesha ustadi wao katika kutumia maneno kisanii ili kuwasilisha ujumbe
kwa wasomaji au jamii lengwa
Mulokozi(1989)anasema kuwa fasihi ni sanaa itumiayo lugha ili
kufikisha ujumbe kwa jamii bila kujali kuwa imeandikwa au haijaandikwa.
Kutoka na maana ya fasihi kwa wataalamu hao,tunaweza kusema kuwa fasihi
ni aina ya sanaa ambayo hutumia lugha katika uwasilishaji wake kwa hadhira
lengwa bila kujali kuwa imeandikwa au haijaandikwa ili kufikisha maudhui kwa
hadhira lengwa au iliyokusudiwa.
Oruka (1990), na Mbiti (2011).
Wameifafanua dhana hii ya falsafa ya
kiafrika kuwa ni fikra au mitazamo wanayoishughulikia waafrika wenyewe au watuwengine ambao
wanakubali mila na desturi za kiafrika.
Hivyo twaweza sema kuwa falsafa ya
kiafrika ni dhana au mawazo ya waafrika wenyewe juu ya mambo mbalimbali wanayoyafanya kama
vile imani juu ya maisha, mila, desturi,jinsi ya kushirikiana katika katika
jamii, na kutafuta suluhisho juu ya changamoto au matatizo yanayowakabili. Utambulisho
wa falsafa ya kiafrika, sifa hizo ni kama vile; falsafa ya kiafrika imejikita
katika tanzu za fasihi simulizi,
Mfano
a) visasili;
b) visakale.
c) Sifo
d) Ngano
e) Mafumbo
f) Vitendawili
g) Miviga
h) Ngomezi
i)
Tambiko
j)
ngoma.
Wamitila, (2004).Anaeleza kuwa haipingiki kuwa falsafa ya kiafrika hujidhihirisha katika
tanzu za fasihi simulizi ya Kiswahli. Tanzu zifuatazo zinathibitisha uwepo wa falsafa ya kiafrika miongoni mwa tanzu hizo
ni kama zifuatazo;
Falsafa ya kiafrika inajidhihirisha
katika
Hadithi;
hadithi simulizi ni masimulizi
ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au
sahili.
(Wamitila, 2003). Anaeleza aina za
hadithi kama vile ngano, visasili, visakale, hekaya, na nyingine nyingi. Kwa
kiasi kikubwa falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika hadithi. Kwa mfano
katika hadithi ya Abunuasi’Katika hadithi hii Abunuasi alikufa kirahisi baada
ya kutolewa nguvu uhai ambazo zilitolewa kwasababu ya ujinga wake kuto tumia
akili zake.
Falsafa ya waafrika inajitokeza
kupitia ushairi wa fasihi simulizi,Waafrika wana mfumo maalumu wa fikra na
hujishughulisha na mila, desturi, tamaduni, na namna ya kutatua matatizo yao.
Msanii anadhihirisha waziwazi
falsafa ya kiafrika anapozungumzia masuala ya
i.
Ndoa
ii.
saula
iii.
dini
iv.
suala
la maadili
v.
suala
la malezi ya familia.
Haya ni mambo yaliyopo na
yanayotokea katika jamii yetu ya kila siku. Mwanafalsafa wa kiafrika “
Tempeles” anasema falsafa ya kiafrika imejikita katika mila, desturi, na
tamaduni za kiafrika. katika wimbo huu kutokana na tamaa mbaya vijana wanakiuka
maadili na kutowajali wazazi wao, wamewaacha marafiki, ndugu, wake, na watoto
pia. Sababu ya tamaa wamesahau amri za mungu kuwa usiue. Usiibe, usitamani vya
watu, pia waheshimu baba na mama yako. Mwisho wa tamaa ni kifo na kupelekwa
gerezani. Hivyo basi msanii anaamini na anaonya kuwa mwisho wa tamaa ni majuto
tuache tamaa.
Falsafa ya kiafrika katika semi,
semi ni tanzu ya fasihi simulizi ambayo hujishughulisha na maneno yasiyokua na
majibu ya moja kwa moja kwa msikilizaji ama hadhira. Katika utanzu huu kuna
vipera vinavyo ambatana nacho, baadhi ya vipera hivyo ni misemo, nahau,
mafumbo, na lakabu.
Semi ina dhima zake katika jamii
inapotumika na baadhi ya dhima hizo ni kama vile kuelimisha jamii juu ya mambo
mbalimbali mazuri ya kufanya, kama kusikiliza kauli njema za wakubwa wetu na
wazazi, mfano msemo wa “asiyefunzwa na mamae hufunzwa na ulimwengu”.”asiye
sikia la mkuu huvunjika guu”.
Kwa upande mwingine semi hizo kuonya
na kuadabisha jamii juu ya mambo mbalimbali mabaya na yasiyofaa katika jamii,
kama wizi, imani na tabia mbaya, mfano msemo usemao “za mwizi ni arobaini”.
Semi ni miongoni mwa tanzu za fasihi simulizi inayoonesha falsafa ya jamii moja
na nyingine. Wanafasihi wana dhihirisha kuwa falsafa ya kiafrika inaweza
kujidhirisha katika utanzu huu wa semi kwa kupitia vipera mbalimbali vya utanzu
huu.
Kwa
mfano, kupitia methali mbalimbali zinazotumika katika jamii ya waafrika
dai hili linaweza kuthibitishwa,kwa kutumia mifano ya methali zifuatazo; asiye
na mwana aeleke jiwe.”, “Mgaagaa na upwa hali wali mkavu”, na “Ndondondo si
chururu”Aliye juu mngoje chini”. Falsafa ya Afrika inadhihirisha kuwa katika
masuala ya utawala, waafrika walikuwa katika makundi madogo madogo kama vile
koo au makabila, na mtu aliyekuwa anaaminika kuwa ni mwenye nguvu ndiye
aliyekuwa anatawala katika jamii husika. Viongozi waliokuwa wanaaminika kuwa ni
wenye nguvu ni kama vile; chifu Mkwawa, Kinjekitile Ngwale, na Chifu Mangungo
wa Msovelo.
Falsafa ya kiafrika ikijidhihirisha
katika sanaa za maonesho; katika kujadili vipengele vya ujidhihirishaji wa
falsafa ya kiafrika, tumechagua vipera viwili katika utanzu huu ambavyo ni
a) Kupitia matambiko.
b) Kupitia ngoma za jadi.
Matambiko, ni miongoni mwa vipera vya
sanaa za maonesho ambacho wahusika wake katika jamii hufanya shughuli
mbalimbali za kutoa sadaka kwa miungu, wahenga, na mababu waliowatangulia,
ambao wanaonekana wana nguvu asilia zinazosaidia kuepusha utokeaji wa majanga
kama njaa, radi, ukame, mafuriko, kuvamiwa au kutekwa kwa utawala, pamoja na
kushinda vita. Katika jamii ya wabena, matambiko mbalimbali hufanywa ikiwemo
matambiko yanayofanyika mtu anapo kosa motto ama kukosa kutunza mali za urithi
wa wazazi wake.
Shughuli mbalimbali wakati wa
matambiko hufanywa mfano ngoma, nyimbo na sherehe zinazoambatana na wanyama
kuchinjwa na damu zao kutumika kama sadaka kwa ajili ya matambiko hayo. Katika
kuthibitisha hili Placide Temples anaeleza kuwa maisha ya jamii nyingi za
wabantu wanategemea nguvu uhai (vital force) ili kujikinga na utokeajia wa
majanga katika jamii hizo kama ilivyoneshwa katika jamii ya wasukuma.
Ngoma; hiki ni kipera kinachoonesha
utokeaji wa falsafa ya kiafrika katika maisha halisi ya waafrika wenyewe. Ngoma
katika jamii za kiafrika ni kiashiria cha mambo muhimu, mfano hutumika kama
nembo ya utawala, kitumbuizi katika shughuli mbalimbali kama vile harusi au
kupandishwa cheo.
Lengo kubwa ni kutumbuiza watu na
kujua ubora wa .
Katika kujadili dhana ya falsafa ya
kiafrika Temples anasema kuwa mwaafrika hawezi kuacha asili yake ambayo ndiyo
utambulisho wa utamaduni wake. Kama ilivojidhihirisha katika jamii ya wasukuma ngoma ni moja ya
asili zinazotambulisha utamaduni wa jamii husika.
Baada ya kuangalia falsafa ya
kiafrika inavyojidhihirisha katika tanzu za fasihi simulizi. Pia falsafa ya
kiafrika inajidhihisha katika tanzu za fasihi andishi ya Kiswahili kama
inavyoelezewa katika vipengele vifuatavyo;
Falsafa ya kiafrika inajidhihirisha
katika ushairi; ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa
maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari au ishara
katika usemi, maandishi au maadhi ya wimbo (Mulokozi na Kahigi, (1979). Kwa
kutumia “Kunga za Ushairi na Diwani yetu” iliyoandikwa na Kahigi na Mulokozi
falsafa ya kiafrika inajidhihirisha kama ifuatavyo;
Waafrika wanaamini katika suala la
umoja; toka awali waafrika walikuwa na umoja waliishi kwa kushirikiana na hata
kufa nya kazi pamoja kwa manufaa ya jamii nzima. Kwa kuumia shairi la “Msiba
Uliotuangukia” suala la umoja kama imani ya waafrika linajidhihirisha;
“…Na mara shambulio
tukalianza
Huko sauti za
chuki tunazipaza
Tobaa litumbo la
nduli kafiri
Atakaye tumbole
lituhasiri!
Tukalichoma
tukalikata sana…”
Shairi hili linaonesha kuwa waafrika
waliamini katika umoja kama nyezo ya kupinga ukoloni na unyanyasaji. Pia
waafrika wanaamini kuwa wazee ni watu wenye busara, hekima, na mawazo mazuri
ambapo ni vyema kuheshimu mawazo yao. Mfano katika shairi lifuatalo;
Ya Allahu ya Azizi,
unifungulie njia,
“
Nienzi wangu wazazi, nisije kuwakosea,
Waniridhie wazazi, kila nitowatendea,
Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia’.
Suala la kifo; vilevile waafrika wanaamini kifo sio mwisho wa uhai bali ndio mwanzo wa maisha mengine. Waafrika wanaamini kuwa mtu akifa anaendelea kuishi kati yao ingawa hawamuoni. Hii injidhihirisha katika shairi la “kinjikitile Ngwale ” ambapo mtunzi anasema;
‘…shujaaa..ooooh shujaa..kwa mti wa shamba
mkoloni twamtwanga oooohh,shujaa uishi
milele,uishi
milele.
Waafrika wanaamini kuwa watu walio
kufa wapo karibu na Mungu na wale walio hai humuomba Mungu kupitia wale
waliokufa. Hili linajidhihirisha kupitia urithishaji wa majina pamoja na
matambiko au kuomba mizimu ya mababu
inayofanywa na waafrika wengi katika maisha ya kila siku.
Dhana
ya uzuri na ubaya pia imejidhihirisha kama falsafa ya kiafrika hasa katika
shairi la ‘Pendo”. Mtunzi wa diwani hii anadokeza kuwa uzuri au ubaya upo
katika macho ya muonaji au anayeangalia, anasema;
1
moyo wangu ume lizi, mimi kuku penda wewe,
mwingine tena siwazi,sije nitia kiwewe
nina muomba mwenyezi,maisha nikae nawe
pendo langu mimi nawe halihitaji hirizi
2 haliihitaji hirizi,naomba sana welewe
nikumbatie mpenzi,usi hofu wenginewe
wabaki na simulizi,watuige wapagawa
pendo langu mimi nawe halihitaji hirizi
Hii ni dhahili kuwa aghalabu uzuri
au ubaya wa kitu kwa waafrika unategemea na mtazamo au mawazo ya muonaji. Hata
katika jamii mtu anaweza kupenda au kukiona kitu fulani kizuri na mwingine
kukiona kitu hicho ni kibaya.
Katika tamthiliya wandishi
ameonyesha falsafa mbalimbali ambazo zimezoeleka na zinatumika sana na jamii ya
kiafrika. Falsafa zinazojidhihirisha katika tamthiliya hii, ambazo ni kama
vile;
a) Dhana ya ngoma
b) Dhana ya nyimbo,
N.
Hussein na tamthiliya yake ya Mashetani, kuwa ni moja kati ya tamthiliya
za mwanzo kabisa katika harakati za utumiaji wa kanuni za kijadi ndani ya kazi
za kifasihi. Wafura anasema:
“Hussein
alijitokeza tena uwanjani, akathibitisha ameidhibiti bahari ya tamthiliya kwa
kutoa ‘Mashetani”
Katika tamthiliya hii mwandishi
ameonyesha namna ngoma na nyimbo zinavyochukuliwa katika jamii nyingi za
kiafrika. Ngoma na nyimbo huchukuliwa kama ni dhana ambazo zinazochochea umoja
na ushirikiano kwa jamii wakati wa kufanya kazi na mara dhana hizi
zinapokosekana kazi huzorota na hata watu huvunjika moyo na kushindwa kufanya
kazi, na mwisho hutawanyika.
Mwandishi “Hussein”ametumia ngoma na
nyimbo kama kichocheo cha kufanya kazi.Hivyo huu ni uhalisia uliopo katika
jamii za kiafrika hususani kwenye makabila mbalimbali, ngoma na nyimbo
huchukuliwa kama vichocheo na viashiria vya matukio ndani ya jamii.
Dhana ya mwanamke katika jamii,
mwandishi Medical aid foundation ameonyesha
namna mwanamke anavyochukuliwa na jamii Mwanamke
amechorwa kama mtu asiye na elimu juu ya mambo ya jinsia na ukimwi, katika
kuilezea nafasi hii, mwandishi anamtumia muhusika Mama Suzi, ambaye anaoneka kutokuwa
na ufahamu mzuri juu ya masuala ya UKIMWI, kwa mawazo yake anaamini kuwa
ugonjwa wa UKIMWI ni ugonjwa unaowahusu watu wakubwa tu, na watoto hawawezi
kuambukizwa jambo ambalo si sahihiVile
vile, mwandishi amemchora mwanamke kama chombo cha starehe, anamtumia
muhusika Joti ambaye anawatumia wanawake ili kujistarehesha kingono, lakini pia
tunaona namna watu wanavyotumia pesa na vitu vya thamani ili kuwarubuni
wasichana wapate kukidhi mahitaji yao ya kingono.
Jambo hili lipo miongoni mwa jamii
za kiafrika ambapo mwanamke anachukuliwa kama kiumbe duni asiyeweza chochote
mbele ya mwanaume na ndio mitazamo ya wanaume na wazee katika familia nyingi za
kiafrika,kwa mfano mtoto wa kike mara nyingi hutengwa na mtoto wa kiume katika
shughuli mbalimbali likiwemo suala la elimu.
Kwa hiyo mwandishi ameonyesha namna
gani falsafa ya kiafrika inavyojidhihirisha juu ya anavyochukuliwa mwanamke,
tofauti na Ulaya na Asia ambapo mwanamke amepewa nafasi kama mwanaume katika
Nyanja zote za kimaisha.
Pia kupitia riwaya ya “Mirathi ya Hatari”
iliyoandikwa na Mung’ong’o,G. tunashuhudia falsafa ya kiafrika inajidhihirisha
katika vipengele vifuatavyo kama ifuatavyo;
Kifo,
waafrika walio wengi mbali na
kuamini kuwa vifo vingi vinavyotokea katika jamii vina sababu zake ambazo
huelekezwa katika Mungu na uchawi au ushirikina. Haya yamezungumzwa na
wanafalsafa wa kiafrika kama vile Placide Temples na Samweli Mbiti. Katika
riwaya hii hali hii inajidhihirisha kupitia kifo cha mzee Kazumbe.Cchanzo cha
kifo ni kulogwa, mwandishi anasema “Mwanangu, leo asubuhi nilikwenda kwa mama
Tumwene kuulizia kifo cha baba yake Uganga unasema kuwa kifo chake kimetokea si
kwa mapenzi ya Mungu, ila kwa michezo ya binadamu wafaidio kuwaona watu wakifa!
Katika tamthiliya ya Lina Ubani tunaambiwa kuwa Talafa aliyekuwa
msumbufu kwa wanakijiji walioktiwa wamelima fiwi badala ya pamba aligeuzwa
shingo, uso umetazama mgongoni! Jambo hili ni la kutisha. Linaweza kubadilisha
nia ya afisa yeyote mtendaji ambaye atakwenda kijijini hapo.
Pia suala la dini, kupitia
mwanafalsafa John Samweli Mbiti ni dhahiri kuwa waafrika wana dini zao tangu
mwanzo mbali na ujio wa wakoloni ambao walileta
ukristo pamoja na uislamu wao. Katika riwaya hii mwandishi kupitia
wahusika kama Gusto na mama yake (Nyamidze) ni wakristo tena huwa wana kwenda
kanisani katika (uk 29) baada ya Gusto kuoga na kuvaa ili aende kanisani
anamuuliza Nandi, “Hivi mama amekwenda wapi?” Nandi anajibu “Amekwenda
kanisani”. Ni usiku huo huo tu wa kucha jumapili Gusto alihudhuria kikao cha
wachawi mapangoni.
Siku hiyo hiyo ya Jumapili mama yake
Gusto (Nyamidze) anaenda kwa mganga (uk 37) kwa mama Tumwene. Huu ni uhalisia
katika jamii zetu, matatizo yanapoikumba familia za watu mbalimbali miungu
hukimbiliwa. Uamini kuwa mtu akifa hujiunga na miungu.
Suala la urithi, katika falsafa ya
kiafrika tunaamini mzazi hasa baba anapofariki huwaachia urithi watoto wake
hasa wa kiume. Katika “Mirathi ya Hatarianasema
‘Nakuachia dawa zote na milki yangu
katika mizungu ya sihiri”. Mirathi hii anaipokea Gusto na baadaye inasababisha
madhara makubwa ikiwa ni pamoja na vifo vya mama, dada, na hata kipenzi chake
Dina ambapo vifo vimetokea kama kisasi baada ya Gusto kumtoa kafara mjomba wake
Kapedzile. Suala hili la urithi lipo na linajidhihirisha katika jamii zetu za kiafrika.
Kwa kuhitimisha, tunaweza sema kuwa
falsafa ya kiafrika imejikita hasa kuelezea mfumo mzima wa maisha anayoishi
mwaafrika na ukweli kuhusu fikra, mila, utamaduni, na mienendo yake katika
jamii. Kwa sasa falsafa ya kiafrika imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na falsafa ya
kimagharibi hususani suala zima la utandawazi.Kuna mambo mbalimbali kama vile, mavazi, vyakula,dini,
mfumo wa elimu na afya vyote vimebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuzuka
kwa utandawazi. Pia maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesababisha falsafa ya
kiafrika kwa kiasi kikubwa kupotea, mfano ngoma za jadi katika kizazi hiki
zinazidi kupotea kutokana na kuibuka kwa taaluma ya muziki kutoka katika iamii
za kimagharibi.
MAREJEO.
Kahigi, K.K., & Mulokozi, M.M.
(1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzani Publishing
House.
Mbiti, J. (1990). African Religion
and Philosophy. New York: Praeger Publisher
Muhando, P. (1982). Nguzo Mama. Dar
es Salaam: Dar es Salaam University Press
Mung’ong’o, C.G. (1977). Mirathi ya
Hatari. Dar es Salaam: Tanzania publishing House
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya
Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publications
Mulokozi, M.M. (1989) Tanzu za Fasihi Simulizi Mulika 21:1-24,
Dar es salaam: TUKI.
Mulokozi, M.M. (1996) Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu Huria
cha Dar es salaam
Wamitila, K.W.(2002) Uhakiki wa Fasihi Misingi na Vipengele
Vyake. Nairobi, Phoenix,
Publishers Ltd.
Comments
Post a Comment