Umilisi katika lugha ya kiswahili,faida za umilisi,Dhana ya utendaji, Mambo ya kuzingatia katika utumizi wa lugha,umbo la ndani na umbo la nje la sentensiDhana ya sarufi zalishi,maana ya sarufi
Kazi hii imegawanyika
katika sehemu kuu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao unahusisha fasili
za sarufi na sarufi zalishi, sehemu ya pili kiini cha swali na sehemu ya tatu
ni hitimisho.
Dhana ya sarufi
imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo:
Sarufi ni sayansi ya muundo wa lugha pamoja na sheria
na kanuni za matumizi yake ambayo kwa kawaida hukubalika kwa watumiaji wake
(Pei na Gaynor, 1969:88)
Sarufi ni taaluma ya lugha inayohusu uchunguzi na
uchanganuzi wa kanuni na vipengele mbalimbali vya lugha (Massamba na wenzake,
2004).
Sarufi ni sayansi ya muundo wa lugha pamoja na
sheria, kanuni na matumizi yake ambayo kwa kawaida hukubalika kwa watumiaji
wake(Kihore 2012).
Sarufi ni kanuni na sheria au taratibu za uchambuzi
zinazotawala lugha(Massamba na wenzake, 2001).
Sarufi ni utaratibu wa kanuni ambazo humwezesha
mtumiaji wa lugha kutunga tungo sahihi zinazoeleweka mara zinapotamkwa
(Kapinga, 1983).
TUKI, (1999) Sarufi ni sayansi ya lugha.
Kutokana na fasili za wataalam hapo juu sarufi ni taratibu
na kanuni zinazotumika katika kuunda lugha kwa kuzingatia ukubalifu wa
watumiaji wake huku ikizingatia viwango vyote vya uchambuzi yaani kiwango cha
maana,matamshi, miundo, na maumbo katika lugha husika.
Sarufi zalishi ilizuka kutokana na kasoro za sarufi
mapokeo na sarufi miundo katika uchanganuzi wa lugha. Mtazamo huu uliasisiwa na
Noam Chomsky katika kitabu chake cha syntactic structurecha mwaka (1957).
Mtazamo wa sarufi zalishiulijikita katika uundji wa nadharia ambayo ingeeleza
namna lugha hutumiwa na watumiaji wake hususani, jinsi wanavyotumia kanuni
chache katikalugha yao kuzalisha sentensi nyingi na zisizo na kikomo. Kutokana
na uwezo huu mzawa wa lugha huweza kuunda tungo ambazo ni sahihi na ambazo si sahihi
(Matinde,2012).
Chomsky, amewasilisha mtazamo wa Sintaksia
unaotambuliwa kama Sarufi zalishikatika
kaziyake.Chomsky alikusudia kukuza fafanuzi mwafaka za hali ya sintaksia ya
lugha mbalimbali,yaani jinsi lugha mahususi zinavyounganisha maneno kuunda sentensi.Vile
vile kazi hiyo ilidhamiria kukuza nadharia ya kijumla ya sintaksia
inayobainisha ni mambo yapi ya kijumla yanayopatikana katika lugha mbali mbali
na jinsi gani masualahayo yanavyotofautiana katika uwanja huu wa sintaksia.
“In linguistics, generative grammar is a grammar (or
set of rules) that indicate the structure and interpretation of sentences which
native speakers of a languages accept as belonging to the language”
Sarufi zalishi ni sarufi mkusanyiko wa kanuni
inayoonesha muundo na tafsiri ya sentensi ambayo mzungumzaji wa lugha (mzawa)
au mmilisi wanavyo ipokea kama ilivyo.
Dhana za msingi
za nadharia za sarufi zalishi;
Umilisi, ni ujuzi
au uelewa wa kanuni zinazotawala lugha fulani ambazo kila mzungumzaji wa lugha
asilia huwa nao. Ujuzi huu huhodhiwa ubongoni mwa mzawa wa lughana ndio
humwezesha kutunga tungo nyingi na zenye urefu wowote.
Ujuzi huu huhusu kanuni
zinazotawala lugha hiyo husika. Ujuzi huu humwezesha kutambua sentensi sahihi,
zisizo sahihi na kupambanua sentensi zenye utata. Pia humwezesha kupuuza makosa
katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, na kukatisha sentensi.
Chomsky anaeleza kuwa mtu anapojifunza lugha huanzia na umilisi na
anaendelea kudai kuwa kwa kiasi kikubwa umilisi wanaokuwa nao wazawa wa lugha
moja hufanana na hii ndiyo inayowafanya waelewane katika mazungumzo yao kwamba
mzungumzaji anasema kile anachotaka kusema na msikilizaji anaelewa kile
kilichosemwa na msikilizaji.(Rubanza,2003).
Umilisi humwezesha mzawa wa lugha;
Ø kutambua
sentensi sahihi na ambazo si sahihi mfano:
i)
(Sahihi) Mwalimu anafundisha wanafunzi
darasani.
(Si
sahihi)Wanafunzi anafundisha mwalimu darasni.
ii) (Sahihi)
Mtoto mdogo anaimba.
(si
sahihi) Anaimba mdogo mtoto.
Ø Kutunga
sentensi nyingi zenye urefu wowote :
i)
Msichana mrembo mrefu mweusi alikamatwa
bustanini jana jioni, akiiba matunda ya mzee Juma na kupelekwa kituo kidogo cha
polisi kwa maelezo zaidi.
ii)
Mtoto mdogo aliyeanguka jana jioni na
kuvunjika mkono, amepelekwa hospitalilakini bado hali yake ni mbaya hivyo
madaktari wameamua kumpeleka hosipitali ya mifupa kwa uchunguzi zaidi ili
kupata suluhisho la tatizo lake.
Ø kutambua
sentensi zenye maana sawa.
Mfano;
i)
Watoto wanakula chakula.
Chakula kinaliwa na watoto.
ii)
Mama anapika chakula.
Chakula kinapikwa na mama.
Ø kutambua
sentensi zenye utata, mfano;
i)
Juma amenunua mbuzi.
Utata
upo katika neno mbuzi lenye maana zaidi ya moja.
Mbuzi
kama kifaa cha kukunia nazi
Mbuzi
kama mnyama.
ii)
Mama ana paa.
Utata
upo katika neno paa lenye maana zaidi ya moja.
Paa
kama kitendo cha kukwea juu ya, mfano mti, mlima, angani.
Paa
kama mnyama aishie polini.
Ø Kutambua
muundo wa tungo katika lugha yake na vipashio vyake.
Mfano;
i)
Mbunnge wetu amewasili jimboni.(Tungo
sahili)
ii)
Kitabu kilichopotea kimepatikana. (Tungo
changamano).
Ø Kutambua
aina mbalimbali za sentensi katika lugha yake
Mfano;
i)
Mwalimu anafundisha Kiswahili. (Sentensi
arifu).
ii)
Shika chini. (Sentensi amrishi).
iii)
Wanafunzi wangapi wamefika? (Sentensi
ulizi).
iv)
Mapunda, na wewe umefika! (Senteansi
mshangao).
v)
Lugano angalikuja mapema angalimkuta
Amiri. (Sentensi shurutia).
Ø Kutambua
sentensi zenye maana na zile zisizo na maana.
Mfano;
i)
Baba analima shamba.
ii)
Shamba analima baba.
Hivyo ili kutambua sentensi zenye maana na zile
zisizo na maana, kulingana na muundo wa sentensi za kiswahili,
muundo wa sentensi zilizopo katika mfano wa pili si sahihi kwani zimekiuka
sintaksia ya lugha yaKiswahili.
Utendaji ni dhana mojawapo ya
sarufi zalishi, hurejelea usemaji na utumizi wa ujuzi wa mzawa wa lugha katika
kutumia lugha yake ndani ya muktadha wa lugha mahususi. Utumizi huu wa lugha
huzingatia :-
·
Muktadha:
Mifano,
- Kaniletee
chaki ofisini (shuleni)
- Nani wa
kuondoka? (stendi).
- Amependeza
hajapendeza? Bibi kampata bwana na bwana kampata bibi ( ukumbini).
·
Uhusiano baina ya wahusika,
Mifano;
Mchungaji na waumini;
Mchungaji: Bwana Yesu asifiwe.
Waumini: ameeeen.
Mchungaji: leo bwana amenionesha
Waumini: ameeeeeni.
Mzazi na mtoto
Mzazi: Amina leo
mmejifunza nini shuleni?
Mtoto: Tumejifuna kiswahili mama.
Mzazi: Vizuri mwanangu,
sasa kabadilishe nguo chakula kiko jikoni,
alafu uoshe vyombo.
Mtoto: Sawa mama.
Hakimu na
mshtakiwa.
Hakimu:
Mshtakiwa una lolote la kujitetea?
Mshtakiwa:
Ndio mweshimiwa hakimu.
Hakimu: Jitetee.
Mstakiwa:
Mheshimiwa naomba mahakama inipunguzie adhabu kwa
sababu nikosa langu la kwanza pia nina familia
inayonitegemea.
Daktari na
mgonjwa.
Daktari:
Meza mbili kutwa mara tatu
(2×3×7)
Mgonjwa:
Sawa daktari.
Daktari:
Hakikisha unakunywa maji ya
kutosha.
Mgonjwa:
Sawa daktari.
Hivyo basi katika utumizi wa lugha uhusiano baina ya
wahusika huwawezesha kuteua aina ya mazungumzo yanayostahili kulingana na
mazungumzo husika.
Mada ya mazungumzo
Mfano;
Mada ya kisiasa.
Kiongozi: “People’s”
Wananchi: “Power”
Kiongozi: Leo ni siku pekee ya kuzungumza na
wananchi, naomba
mniskilize kwa makini.
Mada ya afya.
Bwana afya: Ndugu
zangu chimbeni mashimo ili tuondokane na magonjwa ya
kuambukiza kama yanayojitokeza katika kijiji
chajirani.
Wanakijiji: Sawa
mkuu, tutatekeleza.
Dhumuni la
mazungumzo.
Mfano;
Dhumuni la kuelimisha;
Mshauri
nasaha: Kutokana na majibu ya vipimo
vyako, inabidi ule vizuri chakula bora
ikiwa ni pamoja na matunda,pia upate muda wa
kupumzika.
Ukizingatiahaya
utaishi kwamatumaini.
Mgonjwa: Sawa.
Dhumuni la kuonya.
Mazungumzo kati ya mzazi na mtoto:
Mzazi: Siku hizi umekua ukichelewa kurudi
nyumbani, kinachokuchelewesha
nini?
Mtoto: Usafiri
mama.
Mzazi: Usafiri
gani huo mpaka saa nne za usiku? mbona
Aisha amewahi
kurudi?
Mtoto: (kimya).
Mtoto: (kimya).
Mzazi: Mwanangu
dunia haiko hivyo unavyodhani, umebadilika sana siku hizi. Ujana
una mambo mengi, ni vyema uutumie ujana wako vizuri, kumbuka kuna
magonjwa hatari
na yasiyotibika.
Dhumuni la kuburudisha:
Mfano;
Mshereheshaji na wageni waalikwa:
Mshereheshaji: Piga
vigelegele kwa maharusi wetu jamani.
Wageni waalikwa: Kilililiiiiiiiiiiiii
………………..
Mshereheshaji: Mwenye
wivuuuuu…………...
Wageni waalikwa:
Ajinyongeeeee ……………….
·
Jinsi.
Tofauti za kimaumbile baina ya ke na me hupelekea
wazungumzaji wazawa wa lugha kuteua aina fulani ya lugha ya mazungumzo kutokana
na jinsi zao.
Mfano;
Mazungumzo kati ya mwanamke na mwanamke:
Asha: Mambo
shosti?
Getrude: Safi
tu shoga angu.
Asha: Nakuona
umepodoka si mchezo?
Getrude: Mambo
ya mfikemo hayooo ………..
Mazungumzo kati ya mwanaume na mwanaume,
Juma: Nambie
kamanda.
Hamisi: Poa jembe langu.
Juma: Ishu zinaendaje?
Hamisi: Burudani, kuchakarika tu.
Hata hivyo utendaji huweza kuathiriwa na kasoro za
kimatamshi, hasira, furaha, uchovu,ulevi na matatizo ya kumbukumbu.
Umbo la ndani.
Katika umbo hili hujitokeza katika sentensi kabla
haijafanyiwa mchakato wa kimofofonolojia. Umbo la ndani hubeba maana kamili ya
tungo na vipashio vya tungo hubainika bayana, kwani huwa havijafanyiwa michakato
yoyote.
Sentensi
zifuatazo zina umbo la ndani:
Kitabu
alikionipa.
Mjengi wa
nyumba.
Mpiki wa
chakula.
Baada ya sentensi hizi kuambikwa viambishi
vipatanishi vya kisarufi(baada ya mchakato wa kimofofonolojia) tunapata sentensi ambazo zipo kweny umbo la
nje.
Kitabu
alichonipa.
Mjenzi wa
nyumba.
Mpishi wa
chakula.
Umbo la nje;
Umbo hili hutokea baada ya umbo la ndani kufanyiwa
mageuzi au mchakato wa kimofofonolojia muhimu hadi kufikia kiwango cha usemaji
sahihi na unaokubalika, kwa hivyo umbo la nje hudhihirika kimatamshi na
kiothografia. Umbo hili haliwezi kufanyiwa michakato zaidi.
Mifano,
Umbo la ndani Umbo la nje
Juma
umwa maino. Juma anaumwa meno
Mama piki kiakula.
Mama anapika chakula
Kijana mwibi.
Kijana mwizi.
Uchamko;
Uchamko ni utaratibu wa kutumia sheria fulani ambazo
huweza kutumika mara kwa mara katika kuunda sentensi ambazo zina urefu usio na
kikomo.Uchamko, hutokana na sentensi zaidi ya moja kupachikwa katika Sentensi
ile ya kwanza ili kuunda sentensi moja isiyo na kikomo, uchamko hujitokeza
katika aina kuu mbili, ambao ni utegemezi na uambatanishaji.
Utegemezi;
Uteggemezi ni aina ya uchamko ambao hutokana na
matumizi ya maneno kama: kuwa, kwamba, kama, na ili. Pia hutokana na hali ya
kuwepo au kutokea kwa kipashio kimoja cha kiisimu ambacho hutegemea uwepo wa
kipashio kingine. Utegemezi huweza
kutokana na;
Upachikaji kwa kutumia vijalizi na urejeshi ambao
hutumiwa kuunda sentensi changamano.
Mfano,
Mbuzi aliyechinjwa jana amepikwa leo.











Mbuzi aliyechinjwa jana amepikwa leo.
Uambatanishaji;
Uchamko pia huweza kudhihiriishwa na uambatanishaji
wa sentensi, huu ni uchamko ambao hutokana na sentensi ambbatano.
Mfano,






















Mtoto anacheza baba
analima na
dada anaimba.
Dhana ya mwisho ya sarufi zalishi ni uchamko, uchamko ni utaratibu wa kutumia
sheria fulani ambazo huweza kutumika mara kwa mara katika kuunda sentensi ambazo
zina urefu usio na kikomo. Uchamko hutokana na sentensi zaidi ya moja kupachikwa
katika Sentensi ile ya kwanza ili kuunda sentensi moja isiyo na kikomo. Pia
hutumia kanuni chache kutunga sentensi nyingi zisizo na kikomo. Uchamko
umegawanyika katika sehemu mbili yaani utegemezi na uambatanishaji.
Utegemezi
Ni uchamko ambao hutokana na hali ya kuwepo au
kutokuwepo kipashio kimoja cha kiisimu ambacho kinategemea uwepo wa kipashio
kingine. Utegemezi hutambulishwa na maneno kama vile; ili, kwamba, kama na
kuwa. (Matinde, 2012)
Mfano; Ambakisye
alijua kuwa Ndope anafahamu kuwa shule itafunga kesho.
Asha anajua kuwa mimi najua kuwa atafaulu mtihani.
Uambatanishaji.
Ni aina ya uchamko ambao hudhihirishwa na
uambatishaji wa sentensi sahili mbili au zaidi. Kwahiyo, huu ni uchamko ambao
hutokana na sentensi ambatano.
Mfano;
Shangazi anapika, mama anaandaa chakula na baba
anakula.
























baba
anakula
Kama ilivyo kwa nadharia zingine,
nadharia hii pia ina ubora na udhaifu wake.
Ubora wa nadharia hii.
·
Imeweza kuonesha umilisi alionao
binadamu katika lugha yake, kuwa anaweza kuzalisha tungo au sentensi mbalimbali
kwa kutumia kanuni chache zilizopo katika lugha yake.Umilisi huo humsaidia
mtumiaji wa lugha kuunda sentensi hizo hata kama hajui kusoma na kuandika.
·
Pia nadharia hii inaonesha kuwa kila
mzungumzaji wa lugha huzifahamu vizuri kanuni chache zilizopo katika lugha yake
na kuzitumia kanuni hizi katika kuwasiliana na jamii inayomzunguka.
·
Vilevile nadharia hii ya sarufi zalishi
imeweza kuonesha kuwa binadamu anao uwezo wa kufafanua kipi ni sahihi na kipi
sio sahihi katika uteuzi wa maneno wakati wa uzungumzaji.
·
Nadharia hii inamchukulia binadamu kama
kiumbe chenye uwezo endelevu wa kuzalisha sentensi ambayo inaweza kueleweka kwa
jamii inayomzunguka.
·
Pia nadharia inatuonesha kwamba upo
uhusiano mkubwa kati ya akili, kufikiri na lugha.Hususan katika dhana ya utendaji
mtumiaji wa lugha anatakiwa kutumia akili anapoteua lugha ya kutumia ili
kuendana na muktadha.
Udhaifu wa
nadharia hii.
·
Inafafanua namna au jinsi watu
wanavyozungumza lugha na sio kuwaeleza wazungumze vipi lugha hiyo itumike.
·
Haitilii mkazo mabadiliko katika lugha
hata kama yapo.
·
Vipengele kama umbo la ndani na umbo la
nje vinaweza kumchanganya mtu anaejifunza lugha.
Hivyo ni kweli kwamba nadharia ya
sarufi zalishi imeleta mapinduzi makubwa katika taaluma ya sarufi miundo.
MAREJEO
Kapinga, (2012), Katika Dafina ya Lugha: Serengeti Education
Publishers (T) Ltd, Mwanza.
Kihore Y, M. Massamba, D.P. B na Msanjila,
Y. P. (2012),Sarufi Maumbo ya Kiswahili
Sanifu
(SAMAKISA): TUKI, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Massamba, D. P. B, Kihore, Y, M na
Hokororo, J. I,(2001), Sarufi Miundo ya
Kiswahili
Sanifu(SAMIKISA):
TUKI: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Massamba, D. P.
B, na wenzake(2004),Kamsi ya Isimu
Falsafa ya Lugha: TUKI,
Dar es Salaam.
Matinde, L. (2012),Dafina ya Lugha: Serengeti Education
Publishers (T) Ltd, Mwanza.
Pei na Gaynor, (2012), Katika Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu
(SAMAKISA): TUKI,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
TUKI, (1999), Kamsi Sanifu ya Isimu ya Lugha: Chuo Kikuu cha
Dar er Salaam.
tofauti kati ya dhana za utedaji na umilisi ni zipi???
ReplyDeleteJudikay nerfuler
ReplyDeleteHongera
ReplyDeleteHongera
ReplyDelete