Utata katika maana ya maana na nyanja za kuangalia maana ya maana. Nadharia za maana ya maana na mapungufu yake. Sababu za utata na namna ya kuondoa utata huo.



Utata katika maana ya maana  na nyanja za kuangalia maana ya maana.
Nadharia za maana ya maana  na mapungufu yake.
 Sababu za utata na namna ya kuondoa utata huo.

 Ullman anasema kuwa maana ya maana nimojawapo ya dhana inayo ibua changamoto,hii ni kutokana na maelezo ya namna mbalimbali kutpka kwa wataalamu mbalimbali kama vile wanfalsafa ,wanasaikolojia,wanaisimu kuhusu nini maana ya maana.

Habwe na Karanja (2007:204), Crystal (1987), Matinde (2012), Ogden na Richards (1923), wanakubaliana kuwa neno  maana lina fahiwa nyingi, linaweza kudokeza sababu, kusudi, ishara, urejeleo, maelekezo, ufafanuzi, kufaa na ukweli.
Mifano.
Unamaana gani kuto nipigia
   Maana imetumika kama sababu.
Maingumazito yana maanisha mvua kunyesha.
   Maana imetumika kama ishara.
Mtu huyu hana maana yoyote
  Maana imetumika kama thamani
Maisha yana maana gani.
    Maana imetumika kama ukweli.
Kutokana na utata wa maana ya maana wataalamu wanao shughulikia isimu wamejadili maana ya neno maana kupitia nadharia mbalimbali kama vile ;nadharia ya urejeleo,tumizi,taswira au dhana,vichochea, mwitikio na vijenzi semantiki.

UREJELEO
Matinde(2012)anasema kuwa nadharia ya urejeleo iliasisiwa na wanafalsafa ambao walidai kuwa maana hujitokeza pale palipo na jina na kilejelewa chake.Kwa mtazamo huu maana ya neno ni kitu halisi kinachorejerewa na neno. Maneno ni majina ambayo dhima yake ni kutaja vitu. Kwa mfano,
Neno/kitajo
Kirejelewa.
Wanafunzi
Wa shule ya Wekondari Mbambi
Wakulima
Wa Shamba la ushirika la mwanjengwa


UPUNGUFU
i/ si kilia kiambo au leksimu yenye maana ina kirejerewa chake
. Mfano, katika lugha
   Kuna maneno mengine  ambayo hayana kirejeleo. Kama vile Mungu, upepo, shetani, (dhana).
ii/ Haifanyi kazi kwa maneno yenye uhusiano wa kipolisemia. Kwa mfano Kichwa ni
    leksimu yenye kuchanuza maana nyingi.

iii/ Haifanyi kazi kwa maneno yenye uhusiano wa kihomonomia.Homonomiani hali ya maneno mawili au zaidi kuwa na umbo moja lakini maana zake zikawa tofauti.
 Kama vile k barabara
    Barabara linamaana njia pana ipitwayo na watu.
   Barabara linamaana sawasawa kabisa.
iv/ Haiwezi kufanya kazi katika maneno yenye uhusiano wa kisinonimia, vinyambo
     zaidi ya kimoja (kisawe).
NADHARIA YA DHANA / TASWIRA
Matinde(2012) anasema kuwa taswira ni picha iliyomo akilini mwa mtumiaji wa lugha kuhusu kile kinacho rejelewa.Nadharia hii huchukulia kuwa kila binadamu huwa na picha fulani akilini kuhusu dhana, vitu,jina na hata matukio fulani.Kutokana na nadharia hii maana ya kiashiria hutokana na picha ama taswira inayo husiana na kiashiriwa hicho akilini mwa mwanalugha.Katika nadharia hii huhusisha maneno yaliyo dhahania na maneno yasiyo ya dhahania.
Maneno dhahania ni kama vile;Mungu,shetani,njaa,zimwi,hekima,uongo na jini.
Maneno yasiyo dhahania ni kama ni kama vile mboga na leso.
Maneno hayo hufasiliwa kulingana na picha tofauti tofauti miongoni mwa jamii.

MAPUNGUFU
i)Si bainifu na haiwezi kuchunguzika, kutabili chochote, mwanaisimu hawezi kufanya utafiti wa aina moja.
ii)Nadharia hii haijitoshelezi katika uchanganuzi na ufasili wa maana.Hii ni kwasababu kila mzawa wa lugha huwa na picha tofauti juu ya maneno,vitu dhana au hali mbalimbali.

   

NADHARIA TUMIZI/MUKTADHA.
Mwasisi wa nadharia hii ni  Ludwing Wittgenstein mwaka 1930, ambaye  alitamka kwa mifano mingi ya maneno kuwa maana ya neno ni matumizi yake katika lugha.Msisitizo wake upo katika maana ya neno au kisemo kilichotumika katika muktadha maalumu. Mtaalamu huyu anaona kuwa maana ya neno ni matokeo au athari inayotokana na matumizi. Hata hivyo si muhimu kuuliza maana ya neno bali matumizi yake katika muktadha husika.

Nadharia hii hupinga matumizi ya kamusi katika ufafanuzi wa maana kwakuwa kamusi haioneshi muktadha wa matumizi ya neno husika.
Wananadharia hii wanmeanisha aina kuu tatu za muktadha ambayo ni
Muktadha wa kijamii,usemi na kiisimu.

Muktadha wa kijamii-Hapa katika muktadha wa kijamii maneno fulani huwa na maana katika jamii fulani na yasiwe na maana katika jamii nyingine.
Mfano neno ngariba maana katika jamii inayo jihusisha na ukeketaji na  si jamii ambazo hazifanyi ukeketaji.

Muktadha wa usemi-Huu huongoza uteuzi na matumizi ya maneno mbalimbali
Mifano ;Kula kichwa hicho....muktadha wa kituo cha mabasi.
Muktadha wa kiisimu-maana ya neno katika sentensi hutegemea mazingira ya kiisimu ambamo neno hilo limetumika.
Mfano neno mbuzi
                      Huyu  ni mnyama  anaye fugwa na binadamu.
                      Hiki ni kifaa cha kukunia nazi.
Hivyo maana ya neno mbuzi hutegemeana na muktadha wa matumizi yake.
                     
                               MATATIZO                   
       I.            Inahalalisha tabia ya mabadiliko ya maana kutokana na muktadha.
    II.            Huifanya maana iwe mali ya kundi fulani.


NADHARIA YA VICHOCHEO MWITIKO
Nadharia hii iliasisiwa na  Bloomfield 1933.Nadharia hii imejikita hasa katika kuchunguza maana ya umbo la kiisimu na hali ambamo msemaji hutamka umbo hilo na mwitiko huibuliwa na msikilizaji.Nadharia hii hudai kuwa maana hufafanuliwa kupitia hatua tatu  ambazo ni kichocheo ,tamko na mwitiko.
Nadharia hii huchukulia kuwa maana ni kichocheo cha msemaji na mwitiko wa msikilizaji.
Amina anaumwa kichwa, anaona anaona dawa kabatini(hali ya msemaji) anatamka kuwa anataka dawa. (mwitiko wa msemaji)
          KUUMWA KICHWA                                               ANATAKA
                         ↓                                                                           
              CHOCHEO                                                            MWITIKO


VIJENZI SEMANTIKI/VIKOA VYA MAANA.
Hudai kuwa leksimu zote zaweza kuchanganuliwa kwa kuzingatia seti si ukomo ya vijenzi semantiki ambavyo ni jumla. (Crystal, 1969) uchanganuzi wa vijenzi semantiki ni mkabala uanochunguza leksimu tu.
Mfano  neno ajuza, fahiwa ya leksimu hii ina vijenzi vitatu ambavyo kwa hakika ni;
                                            i.           + Mtu
                                             ii.           +Mzee
                                             iii.          + ke
                                              iv.           -me
                    
Kadhalika vijenzi semantiki huwa na jozi kinzani, jozi hizo huoneshwa kwa alama ya toa na jumlisha. Kijenzi mtu ni cha jumla kinahusisha leksimu hiyo na leksimu kinzani. Leksimu kinzani, mti, majani, vijenzi semantiki vya kijumla kama [MTU], [KITU], [OEVU], hutumika kupambanua leksimu zilizo katika makundi tofautitofauti ya maana.





                               NYANJA ZA KUANGALIA MAANA.

 Matumizi ya maana ya msingi katika kufafanua maana. Hii ndiyo njia kuu ya kulipa neno maana,  ambayo kwa kawaida haibadiliki kutegemeana na athari za kimazingira. Hii inamaana kuwa maana ya neno au tungo itabaki ile ile hata kama mazingira yatabadilika. Maaaana hii ndiyo inayojulikana kama maana ya kileksika. Kwa mfano; kichwa- kikimaanisha sehemu muhimu katika mwili wa binaadamu kinachokusanya viungo kama vile; macho, masikio, pua na mdomo. Hii ndiyo maana pekeyake inayohitaji ulimwengu wa lugha kwa kiwango kidogo sana, hata hivyo bado ulimwengu halisi utahitajika kutokana na matumizi ya maneno kama vile homophoni na homonimia. Mfano neno kama kaa licha ya kuwepo kwa maarifa ya lugha  lakini bado maarifa yaulimwengu halisi yanahitajika kuelewa kusudio la mzungumzaji, kwani yapo mazingira ambayo neno hilo litaendelea kutumika kama kitendo cha kuketi, na mazingira mengine litumike kama cheche la moto, na yote hayo ni maana ya msingi ya neno kulingana na miktadha tofauti tofauti.

 Maana ya ziada au kisarufi. Ni maana abayo huibuka kutokana na maana ya msingi. Maana hii inatudhihirishia kuwepo kwa maarifa ya lugha na wakati huohuo kuna maarifa ya ulimwengu halisi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maana hizi hutegemeana na kuhusiana na mazingira halisi ya matumizi. Kuelewa maana ya ziada sio tu kuelewa maarifa ya lugha, bali pia ulimwengu halisi au muktadha ambapo maneno au fahiwa hizo zimetumika. Mfano pale mzungumzajia atakapo sema “Samahani kaka! Hivi utaendelea kuwa kupe hadi lini? haya ni maisha tu!” utagundua kuwa, hapa kufahamu maana ya tungo hii si kutokana tu na kufahamu maarifa ya lugha, lakini pia inahitajika ufahamu wa ulimwengu halisi ambao tungo hio imetumika, kwa kusema kupe kumaaanisha mtu mnyonyaji au mtegemezi.

Maana ya kimtindo. Hii ni maana inayohusiana moja kwa moja na matumizi ya lugha kulingana na muktadha husika. Katika aina hii ya maana, neno au kiyambo hupata maana kulingana na mtindo ambao neno au kiyambo hicho kimetumika. Mfano mtindo wa kilahaja, mtindo wa wakati, mtindo wa kieneo, au hata mtindo wa taaluma ua fani fulani. Ni lazima tukiri kwamba kuna marifa ya lugha lakini wakati huo huo kuna ulimwengu halisi. Hii ni kwa maana kwamba katika maana hii, lazima mtumiaji wa lugha licha ya kufahamu maarifa ya lugha hio, lakini lazima azingatie ulimwengu halisi ambao lugha hio imetumika. Mfano matumizi ya mtindo wa kilahaja, kuna baadhi ya maneno kiuhalisia huibua hisia zingine na wakati mwingine kushindwa kufahamika kutokana na tofauti za kilahaja. Mfano maneno kama vile, shule, ugali na bomba, maneno haya yanaweza kutumika katika hali tofauti kwa wakaazi wa Tanzania bara na visiwa vya Zanzibar. Kwa upande wa Zanzibar wangeweza kutumia skuli, sembe na mfereji kwa mfuatano. Hivyo basi, kwa mzungumzaji inampasa kujua ni akina nani anazungumza nao na nani wangeweza kumuelewa ingawa wate wana maarifa ya lugha moja.
Aidha, kuwepo kwa maana hisia ni ithibati tosha ya kuthibitisha kuwepo kwa maarifa ya lugha na wakati huohuo ulimwengu halisi katika dhana ya semantiki na pragmatiki zinazohusu maana. Tunapozungumzia maana  ya hisia ni aina ya maana ambayo huibuka kutokana na hisia au mtazamo wa msemaji au mwandishi. Na maana hii huweza kuwasilishwa kwa njia mbalimabali zikiwemo, njia ya maana kama dokezi au njia isiyo ya moja kwa moja. Kwa mfano “kweli wewe ni kidume wa mbegu kwelikweli!” katika tungo hii ni vigumu kufahamu mzungumzaji amemaanisha nini ikiwa msikilizaji hatohusisha maana au kauli hii na ulimwengu halisi au muktadha ambao msemaji au mwandishi amezungumza au kukusudia, kwani maana ya msemaji itakua tofauti na maana ya msikilizaji atakayojengwa kwa kuzingatia tu maarifa ya lugha. Mathalani hapa tunaweza kusema kuwa, msemaji amekusudia huyu kijana ni mchapakazi kwelikweli. Au kwa waswahili wanakawaida ya kumsifia mtu kwa kusema kwa mfamo, huyu mchezaji yaani hafai, mshenzi kwelikweli! Kiuhalisia neno hafai linamaanisha hali hasi ya mtu, vile vile mshenzi ni neno linalotaswira mbaya ya ufedheheshaji, lakini waswahili husema hivyo kuonesha sifa njema za mtu, tofauti n auhalisia. Hivyo kwa mtu kufasiri maana kulingana na maarifa ya lugha inapelekea kupotosha maana iliyokusudiwa.

Maana tangamani. Hii ni maana inayopatikana kutokana na matumizi ya lugha kulingana na muktadha husika wa matumizi kwa kuzingatia maana ya maneno mbalimbali na jinsi yanavyotumiwa kwa pamoja ili kuleta maana iliyokusudiwa. Maana hii pia inatuthibitishia kuwepo kwa maariufa ya lugha na wakati huohuo ulimwengu halisi. Hii inamana kuwa si kujua tu maariufa ya lugha ndio kuweza kuitumia lugha hio, lakini ni kwa vipi lugha hio ingeweza kutumika. Kwa mfano kauli kama vile “Mabibi na mabwana”, mvulan amtanashati, dada mrembo. Ukichunguza tungo hizi utagundua kuwa si kufahamu tu maarifa ya lugha, bali lazima mtumiaji afahamu ulimwengu halkisi wa matumizi ya maneno hayo. Mfano msemaji angeweza kusema, ‘mabibi na mababu” au “dada mtanashati” na ‘mvulana mrembo” jambo ambalo lisengekubalika kajika jamii za waswahili.

Maana mangwi au akise. Ni aina ya maana ambayo huibuka katika hali ambayo maana moja hukonyeza maana nyingine na hivyo humfanya mtu afikirie maana nyingine pia. Mfano kauli “naenda kujisaidia” Katik tungo hii inahitaji mtumiaji wa lugha au msikilizaji kufahamu ulimwengu halisi, yaani  wanajamii fulani wanavyosema kujisaidia wanamaanisha nini? Kwa mfano mara nyingio katika jamii za kiafrika kujisaidia humaanisha ima kuenda haja ndogo au kubwa. Jambo hili katu lisengefahamika kwa sababu tu ya kufahamu maariga ya lugha hio.

Mwisho ni maana ya dhamira au muhimu. Hii ni aina ya maana ambayo hutegemea kile ambacho mtoa ujumbe ana kipa umuhimu zaidi. Mara nyingi kile kinachopewa umuhimu zaidi hutokeza mwanzoni mwa senmtensi. Msingi wa kupata maana katika aina hii inathibitisha kuwa pamoja na kuwa na marifa ya lugha pia panakuwepo n aulimwengui halisi wa lugha. Kupitia aina hii ni vigumu mtu kutambua umuhimu wa msemaji au mzungumzaji kwa msingi tu wa maarifa ya lugha bila kuhusisha hali gani lugha hio imetimika. Mfano kauli ya kusema “Kikwete atashinda uchaguzi wa mwaka 2015” Katika mfano huu umuhimu zaidi upo kwa Kikwete ndiye ambaye ana tarajiwa kushindsa uchaguzi na sio uchaguzi wala mwaka 2015. Haya yote yatabainika ikiwa tu msikilizaji atakuwa anamaarifa ya lugha na wakati huohuo anaujua ulimwegu halisi.
Taaluma ya semantiki huchunduza maana katika viwango vitatu ambavyo ni
a)      Kiwango cha leksia
b)      Kiwango cha tungo/sentensi
c)      Kiwango cha usemi au matini

Maana katika kiwango cha leksia/neno.
Tawi hili huchunguza maana kwa mujibu wa fahiwa zilizopo bila kuhusisha hisia za msemaji au athari za kijamii au muktadha.Tawi hili ndilo hutumiwa katika taaluma ya leksiografia kwani maana ya vidahizo katika kamusi hutokana na fahiwa zilizomo na marejeleo halisi.Hili ndilo tawi kongwe miongoni mwa matawi ya isimu maana.Hii inamaana kuwa neno litabaki lilelile hata kama mazingira yatabadilika.Matinde(2012).
Mfano,
Kichwa – ni sehemu muhimu katika mwili wa binadamu inayokusanya viungo kama vile macho,masikio,pua na mdomo.
Maana katika semantiki/tungo
Hili ni tawi la isimu maana katika kiwango cha tungo hususani sentensi.Huchunguza maana katika miundo mbalimbali ya sentensi.Viwango hivyo ni
a)Anomali/upotoo
Hudhihirishwa na sentensi ambazo matumizi yake yamekiuka matarajio yaani kuna ukinzani wa sifa za maana na mantiki katika sentensi.Hali hii hutokana na mfuaatano wa maneno ambao umekiuka ukawaida katiaka lugha husika.Hapa sentensi ina kuwa sahihi kisarufi  lakini haipo sawa kimantiki.(Matinde,2012).
   Mifano
   Kaka ni mjamzito (kaka hawezi kuwa mjamzito)
   titus ameolewa (mwanaume hawezi kuolewa)
b)Ukinzani
Sentensi mbili husemekana kuwa kinzani iwapo sentensi ya kwanza ama ya pili kuibua maana ambayo inakinzana na maana ya sentensi ya pili au ya kwanza
   Mifano
       I.            Sijui kuimba ila nilialikwa kutumbuiza ukumbini.
    II.            Nilivaa kiatu lakini nikatembea peku
Mifano hii  inaonesha kwamba sentensi zinaonesha sentensi za upande wa kwanza na upande wa pili zinakinzana na umilisi wetu wa lugha na uelewa wetu wa kiulimwengu.
c)Iktisadi
Ikisadi (uwekevu) ni utumiaji wa vipashio vichache katika tungo ama taarifa badala ya kutumia mkururo wa vipashio.Hali hii huweza kurahisisha ufasili na maana iwapo msikilizaji au hadhira inauelewa wa kutosha kuhusu mada ya mazungumzo ,muktadha na dhamira ya msingi.
Mfano
Kwenye usafiri wa daladala ,kondakta anaweza kusem kwa dereva ‘mpe gari hujaona amepiga mkono’.Dereva kwasababu anaelewa dhamira ya kondakta atasimamisha gari ili abilia aingie.
Hivyo ufasili wa kondakta kwa abilia wengine utakuwa mgumu au utaibua utata hii ni kwasababu kondakta ametumia maneno machache na yanayo afiki shughuli husika.
d)Utata
Utata huutokana na sentensi kuwa na maana zaidi ya moja ambayo si wazi na mara nyingi hujitokeza katika viwango viwili ambavyo ni kileksia na kimuundo
Utata kileksia
Huu hutokana na matumizi ya  neno katika sentensi kuwa na maana zaidi ya moja.
Mfano.Mtoto alilalia uji
     Neno lalia lina maana zaidi ya moja ambazo ni
a)      Mtoto alilala juu ya uji
b)      Mtoto alilala akiwa amekunywa uji.
Hivyo itakuwa vigumu kufasili maana sahihi ya sentensi hii bila kuhusisha usemaji huu na muktadha au nia ya msemaji.


Utata wa kimuundo
Ni utata unao jitokeza katika kiwango cha sentensi .Utata huu hutokana na sababu mbalimbali ambazo ni ,
i)Matumizi ya leksimu yenye maana zaidi ya moja.
Mifano.
Kima amekula kima ya kima ya juu.
   Mnyama ,Nyama ya kusagwa  na thamani au kiwango.
ii)Matumizi ya leksimu mbili au zaidi ambayo maana zake si bainifu
Mfano .leksimu zaka na sadaka.
                    Sipendi kutoa sadaka wala zaka
iii) Matumizi ya leksimu ambazo ufasiri wake huibua maana zaidi ya moja (tata)
            Mfano.
Rehema anamiguu mizuri
               Rehema ni mrembo.
               Rehema hutembea kwa kasi.
Johm alimpigia Asha simu.
              Kwaniaba ,kuelekea ama kwakutumia.
iv)Utata unaotokana na mfuatano wa maneno.utata huu hutokana na namna maneno yanavyo pangiliwa katika sentensi.
   Mfano
       Asha amefuga jogoo kumi na tetea.
Hii inamaana kuwa Asha amefuga jogoo kumi na tetea kumi
Misingi ya kuondoa utata
i)Ukweli.
Kwa kuzingatia ukweli wa kiulimwengu,kihistoria,kiisimu ili kuweza kuepusha utata katika ufasili wa maana katika tungo au maneno.
Mfano…………………………………………………………….
ii)Muktadha
Matumizi ya kileksimu,sentensi na usemaji sharti uzingatie muktadha mahususi .Uzingativu huu sharti uende sambamba na usarufi na vigezo vya  mantiki.
Mfano………………………………………………….
iii)Urejeleo
Matumizi ya maneno yanayo onesha urejeleo sharti yawe wazi
mifano…………………………
iv)Ubainifu
Matumizi ya vibainifu vya nomino huweza kuwa utata kama nomono nyingine huweza kuelekeza nomino ileile.
Mifano
             Asha na Happy walinunua gari.
             Asha alinunua hammer na Happy alinunua volkswagen.
Sentensi ya pili ni bainifu kwani haina utata katika tafsiri.
v)Ufasiri/ufafanuzi
Ufasiri/ufafanuzi wa maneno mengine ya kileksimu  ileile ili maana iliyopo iwe wazi kulingana na matakwa au dhamira ya msemaji au mwandishi.
Mifano
      Yule kijana ni mkora anatabia ya kihumi tena jambazi.
      Huyu kiongozi ni mungu mtu,hashauriki na anafanya maamuzi ya ajabu.
v)Uziada dufu
Ni urudiaji wa maneno usio na ulazima wowote.Pia hutokana na matumizi ya maneno mawili au zaidi yenye maana moja.
Mifano.
                Cheusi ni cheusi tu.
                Mwanaume ni mwanaume tu.
vi)Usawe
Ni uhusiano wa kimuundo ambao hudhihirishwa na sentesi mbili kudokeza maana moja.
Mifano.
                            Titus amemwoa trisha
                            Trisha ameolewa na titus
Hivyo sentensi mbili hapo juu zinadokeza maana moja licha ya sentensi hizo kuwa na tofauti kimuundo.



                                                 








                                                             MAREJEO
Alston, W. P. (1967) Meaning The Encyclopedia of philosophy, vol 5 Macmillan  and  Free press,
                                PaulEdwards, Editor in Chief, (pp.233-241), imesomwa tarehe 11/04/2014 saa 22:00
                                kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Baron, J. (1972) Semantic Components and Conceptual development, Elsevier imesomwa tarehe 11/04/2014
                                saa 22:15 kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Bloomfield, W. L. P. (1983) Language, London –New york.

Filp, H (2008) What is Semantics, What is Meaning, imesomwa tarehe 11/04/2014, saa 20:00 kutoka
                                www.sciencedirect.com/science/article.

Habwe, J. na Karanja, P. (2007) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, phoenix publishers LTD, Nairobi.

Holm, P. and Karlgrey, K. (1995) The Theory of meaning and Different perspective on information System,
                                Stockholm University, Marburg.

Lyons, J. (1981) Language; Meaning and Context, Fontana Paperbacks.

Matinde, R. S. (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu,
                               Serengeti Education publishers (T) LTD, Mwanza.

Mdee, S. J. na wenzake (2011) Kamusi ya Karne ya 21: Kamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi Katika Karne
                               Hii, Longhorn publishers LTD, Nairobi.

Sengo, T. S. Y.M (2009) Fasihi za Kinchi, The Regestered Trustees of Al Amin Education and Research
                               Academy, Dar es Salaam.

Wamitila, K. W, (2003) Kamusi: Istilahi na Nadharia, Kenya Focus Publications LTD, Nairobi




Comments

  1. Kazi nzuri saan.Lakini Naomba kujua Nini maana ya uhusiano wa maana kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

notes za malenga wapya,uhakiki wa shairi la malenga wapya.

maana ya sintaksia,uhusiano wa sintaksia na matawi mengine,malengo ya sintaksia au isimu miundo, vipashio vya lugha ni vipi?,

Semantiki kama taaluma nyingine ina mahusiano na taauma nyingine kama ifuatavyo katika mchoro na hatimaye katika maelezo yanayo eleza vipengele mbalimbali vya lugha:-